Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Belle9 ameshangazwa na BASATA kushindwa kulitambua jina lake na kudai kitendo hicho hakina tofauti na baba asiyejua majina ya watoto wake.
Belle 9 amefunguka hayo baada ya BASATA kupeleka orodha ya nyimbo 13 zisizokuwa na maadili kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambazo zina maudhui ambayo ni kinyume na maadili na Kanuni za Huduma ya Utangazaji ya mwaka 2005.
Katika orodha hiyo wimbo wa tatu ni ‘Kibamia’ iliyoimbwa na Roma lakini kwa bahati mbaya jina likaonekana kuandikwa Abernego Damiani a.k.a Roma Mkatoliki ambapo jina hilo ni la Belle9 siyo Roma.
Kupitia akaunti yake Instagram amefunguka na kuandika “Kwa hiyo mimi ni Roma Mkatoliki haya basi ‘Tongwe record’ baby jei mada yo yo yo. Roma Mkatoliki hii ni sawa na kuwa na Baba ambaye akisikia umekosa ana kuhukumu lakini akiulizwa jina la mwanae anaitwa nani anajiuma uma halafu analitaja jina la mtoto wa jirani ambalo huwa analisikia akiwa anakuja kukuhukumu”,.
Jana Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) imezifungia nyimbo 13 kutokana na kukosa maadili katika jamii.