Klabu ya Bayern Munich imefanikiwa kutangaza ubingwa wa Ligi Kuu nchini Ujerumani kwa mara ya tano mfululizo, baada ya juzi kuibuka na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Wolfsburg.

Mabingwa hao wapya wameweza kutangaza ubingwa ikiwa ni saa chache baada ya wapinzani wao kwenye msimamo wa Ligi, Leipzig, kutoka suluhu dhidi ya Ingolstadt na kuwafanya Bayern Munich watangaze ubingwa kwa tofauti ya pointi 10, huku ikiwa imebaki michezo mitatu kumalizika kwa Ligi.

Katika mchezo huo, dakika 45 za kipindi cha kwanza Bayern Munich walikuwa mbele kwa mabao 3-0, yaliyowekwa wavuni na David Alaba, Robert Lewandowski akifunga mawili kabla ya Arjen Robben, Thomas Muller na Joshua Kimmich kuongeza mabao matatu kipindi cha pili.

Kiungo wa zamani wa Bayern Munich, Luis Gustavo, raia wa nchini Brazil ambaye kwa sasa anakipiga katika kikosi cha Wolfsburg, alioneshwa kadi nyekundu kutokana na utovu wa nidhamu na baadaye kutaka kumshambulia mwamuzi.

Kocha wa klabu ya Bayern Munich, Carlo Ancelotti, amejiwekea historia katika klabu kubwa barani Ulaya kutwaa mataji ya Ligi, ikiwa pamoja na nchini Italia, England na Ufaransa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *