Mbunge wa jimbo la Nzega Mjini, Hussein Bashe amesema ametumiwa ujumbe wa vitisho kuwa yeye ni miongoni mwa watu 11 waliopo hatarini kufanyiwa vitu vibaya popote pale watakapoonekana ikiwemo kuundiwa ajali.
Bashe amebainisha hayo leo wakati akiomba muongozo Bungeni ambapo alitaka Bunge liahirishe shughuli zake ili kujadili matukio hayo ya utekaji ikiwa ni pamoja na vitisho hivyo na kubainisha kuwa kuna wabunge wengine akiwemo Mbunge wa Geita Joseph Kasheku Musukuma, ambao wamo kwenye orodha ya watu wanaowindwa.
Katika maelezo yake Bashe amesisitiza kuwa Bunge na Serikali haviwezi kulifumbia macho jambo hilo haramu ambalo kwa sasa imekuwa gumzo katika midomo ya watu masuala ya utekaji watu na kuwapeleka kusipojulikana.
“Kuna watu wamenitumia ujumbe kwamba mimi ni kati ya watu 11 waliopo hatarini kufanyiwa vitu vibaya popote pale tulipo. Bunge na Serikali haviwezi kulifumbia macho jambo hili la haramu wakati Watanzania wanatekwa na watu wasiojulikana”.
Aidha Bashe amesema kuwa kikundi kinachohusika na matukio ya utekaji kiko ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa na kwamba hao ndiyo waliohusika na tukio la kumteka msanii Roma Mkatoliki.