Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), limekemea vikali na kutoa onyo kwa wasanii wanaoendele na malumbano, kukashifiana, kutoleana lugha zisizo na staha sambamba na usambazaji wa taarifa na video zenye mwelekeo wa kudhalilishana.
Katika taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Matiko Mniko leo, vitendo hivyo ni kinyume na kanuni ya 25 (i)- (8) ya kanuni za baraza na kueleza kwamba vinarudisha nyuma juhudi za serikali kuleta maendeleo na kukuza uchumi wa wasanii, wadau wa sanaa na taifa kwa jumla.
Taarifa hiyo imesema Basata inaamini kwamba sekta ya sanaa itakuzwa na juhudi za wasanii wenyewe na kuiongeza ubunifu badala ya kutegemea matukio ya kuchafuana.
Katika siku za hivi karibuni, kumetokea vita kubwa ya kuchafuana mitandaoni kati ya msanii Rajab Kahali ‘Harmonize’ na kundi lake dhidi ya Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’ na kundi lake.