Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limemfungulia mwanamuziki wa Bongo fleva, Emmanuel Elibarik ‘Nay wa Mitego’ kuendelea na kazi zake za muziki baada ya kutekeleza adhabu na masharti aliyopewa na Baraza hilo.
BASATA limemfungulia Nay kutokana na kukiri na kujutia makosa yake na kwamba amejifunza na amebadilika na kuthibitisha kutorudia tena tabia ya hapo awali.
Pamoja na mwanamuziki huyo kufunguliwa na kufanya kazi zake za sanaa Baraza hilo linamuweka kwenye uangalizi maalumu ili kuhakikisha kama anaendesha shughuli za sanaa kwa kuzingatia sheria na maadili ya kazi zake.
Nay wa Mitego alifungiwa na Baraza hilo kutokana na kufanya muziki bila kusajiliwa pamoja na kuimba nyimbo zisizokuwa na maadili ambapo nyimbo yake ya “Pale Kati” ndiyo iliyosababisha mwanamuziki huyo kufungiwa.
Vile vile Baraza hilo limetoa wito kwa wasanii nchini kuendesha shughuli za kazi za sanaa kwa kuzingatia sheria, kanuni na masharti ya sanaa ili kuepuka na matatizo yasiyokuwa na ulazima.