Mwanamuziki wa Dansi Tanzania, Nguza Viking maarufu kama ‘Babu Seya’ amesema alipigwa na butwaa baada ya kusikia kwamba aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli amefariki dunia; siku ile ya Machi 17, mwaka huu.

Babu Seya alisema taarifa hiyo baada ya kuisikia usiku hakulala kabisa hadi asubuhi kwa kumuombea na kumfikiria Rais huyo.

Babu Seya alisema alikosa usingizi kutokana na jinsi mzee huyo alivyomtoa jela ambako ni shimo zito lililokuwa limemfunika yeye na familia yake.

Babu Seya anasema anamuona Magufuli kama baba yake mzazi kutokana na kumtoa jela yeye na familia yake baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

Rais John Magufuli Desemba 9, 2017 aliwaachia huru Babu Seya na mwanaye Papii Kocha waliohukumiwa kifungo cha maisha jela.

Msamaha huo unatajwa kuwa historia na hasa kuwasamehe wafungwa wa maisha na wale wa kunyongwa ambapo kwa wa kunyongwa walioachiwa huru ni 61 na wengine walioachiwa huru kutokana na makosa mbalimbali ni 1,821 huku wengine 8,157 aliwapunguzia adhabu zao.

Nguza Viking, maarufu kama Babu Seya na watoto wake watatu walihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa makosa ya kuwabaka na kulawiti watoto wa shule.Mwaka 2010, rufaa yao ilisikilizwa katika Mahakama ya Rufaa na kuwaachia huru Nguza Mashine na Francis Nguza baada ya kuwaona hawana hatia katika makosa yote waliyoshitakiwa.

Baada ya rufaa hiyo, Babu Seya na Papii Kocha walipatikana na hatia hivyo kuendelea kutumikia adhabu ya kifungo cha maisha jela.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *