Baba mzazi wa Ben Saanane, Focus Saanane ameiomba Serikali pamoja na vyombo vya dola kusaidia juhudi za kumtafuta mtoto wake kwani juhudi zao zimegonga mwamba na suala hilo lipo nje ya uwezo wao kwa sasa.
Suala la kutoweka kwa Ben Saanane liliibuka kwa mara nyingine wiki hii kiasi cha kutikisa mhimili wa Bunge, kabla ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, hajahitimisha kwa kusema kuwa Serikali inachunguza vitendo vyote vya utekaji.
Kuibuka kwa suala la Ben Saanane kulichochewa na tukio la kutekwa kwa mwanamuziki wa Bongo fleva, Roma Mkatoliki na wenzake.
Wakati Roma na wenzake wakichukuliwa mateka kwa siku tatu na kisha kuachiwa, Saanane tangu atoweke Novemba mwaka jana hadi sasa hakuna yeyote wala chombo cha dola kinachofahamu mahali alipo.
Baba huyo wa Ben ameiomba Serikali kuongeza jitihada za kumtafuta mtoto wao ambaye ametoweka toka mwaka jana.
Pia amesema hadi sasa familia hiyo imejitahidi kufanya uchunguzi wa sababu za kupotea kwa mtoto wao, lakini jitihada hizo hazijazaa matunda na kwamba tegemeo lao kubwa limebaki kwa vyombo vya dola na Serikali kwa ujumla