Mwanamuziki wa Bongo fleva, Ruby baada ya kulikacha Tamasha la Fiesta linaloendelea katika mikoa tofauti hapa nchini ameamua kuelekeza nguvu zake kwenye Tamasha la Mziki Mnene linaloandaliwa na kituo cha Radio cha EFM.
Ruby alikataa kufanya show kwenye Tamasha la Fiesta linaloandaliwa na kituo cha Raido cha Clouds FM kutokana na kutofautiana kimaslai na hivyo kuamua kutoshiriki Tamasha hilo maarufu nchini Tanzania.
Mwanamuziki huyo ni zao lililopatikana na Tamasha la Fiesta ambapo aliibuka mshindi kwenye shindano la Fiesta Diva Supa Nyota na kujiunga na Kampuni ya THT ambayo pia inamilikiwa na Mkurugenzi wa Vipindi na uzalishaji wa Clouds Media Group, Bw. Ruge Mutahaba.
Hapo awali Clouds Fm ilitangaza kumsainisha Rubby kama mshiriki wa Tamasha hilo lakini baada ya mazungumzo yao ya kimaslai kashindikana na mwanamuziki huyo akaamua kutoshiriki kuambatana na wasanii wenzake kufanya show kwenye tamasha hilo.
Kituo cha Radio cha EFM ambacho pia kimezindua tamasha la Mziki Mnene wiki iliyopita kimeamua kumjumuisha Ruby kwenye tamasha hilo ili kutoa radha kwa mashabiki wake ambao watamkosa kwenye Tamasha la Fiesta.
Vituo vya Clouds FM na EFM kwasasa vimeonekana kuwa washindani kuanzia kwenye uzalishaji wa vipindi vyao hadi kwenye burudani na hivi karibuni wamekuwa wakichukuliana watangazaji.