Uongozi wa Jiji la Entebbe nchini Uganda umeifunga Baa ya De ambayo mwanamuziki Mowzey Radio alijeruhiwa wiki mbili zilizopita.
Mwanamuziki huyo alifariki dunia jana katika Hospitali ya Case alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kupasuka fuvu la kichwa kutokana na ugomvi kwenye Baa.
Mbali na kuchukua hatua hiyo, Meya Kayanjana ameagiza apelekewe vibali vyote vya baa hiyo ikiwamo leseni na kuwekwa makufuli katika milango yote.
Hata hivyo, ameonya kuwa endapo mmiliki wa baa hiyo atakaidi amri hiyo ya kutoendelea na uendeshaji atatozwa faini ya Sh1milioni za Uganda ambazo atapaswa kuzilipia kupitia Benki ya Stanbic, Tawi la Entebbe.
Katika hatua nyingine, watu wameonekana kuzidi kumiminika katika ukumbi wa Taifa wa maonyesho ambako wananchi watauaga mwili kabla ya maziko yatakayofanyika kesho saa 10 jioni Kaga, Barabara ya Entebbe.
Mwanamuziki Radio aliyewahi kutamba na kundi la Goodlyfe alilazwa katika Hospitali ya Case baada ya kushambuliwa katika ugomvi uliotokea wiki mbili zilizopita katika Baa ya De.