Kesi inayowakabiri viongozi wa juu wa klabu ya Simba, Evans Aveva na Geofrey Nyange ‘Kaburu’ imehairishwa kwa mara nyingine tena hadi Oktoba 4 mwaka huu kutokana na jalada lao bado lipo kwa DPP.
Wakili wa serikali, Vitalis Peter amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa kuwa kesi hiyo imeitishwa kwa ajili ya kutajwa lakini jalada la kesi bado lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili aweze kuangalia kama ameridhishwa na kesi hiyo ama laa.
Kutokana na hayo, Hakimu Nongwa ameahirisha kesi hiyo na sasa itasikilizwa Oktoba 04, 2017 ambapo jalada la kesi hiyo huwenda likawa limeshatoka kwa DPP.
Evans Aveva na Geofrey Nyange ‘Kaburu’ wameshtakiwa na TAKUKURU kwa tuhuma za kughushi nyaraka za Klabu ya Simba na kutakatisha dola za Marekani 300,000 (zaidi ya Sh milioni 650) na wamekuwa rumande tangu Juni 29, mwaka huku wakiwa na safari za kwenda na kurudi Mahakamani kwa kile kinachodaiwa kuwa upelelezi haujakamilika na sasa hivi jalada kuwepo kwa DPP.