Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) itasitisha safari zake kati ya miji ya Dar es Salaam na Songea kuanzia Jumamosi kutokana na ubovu wa njia ya kurukia ndege katika Uwanja wa Songea, imeelezwa.
Taarifa ya ATCL iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana ilisema safari hizo zitarudishwa mara tu baada ya kukamilika kwa matengezo makubwa ya uwanja huo “yanayotazamiwa kuanza hivi karibuni.”
Taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Injinia Ladislaus Matindi ilisema kusitishwa kwa safari za Songea kutakuwa na athari mbili.
Ilisema ukiacha adha kwa abiria wanaokwenda Songea, hatua ya ATCL hiyo pia itaathiri safari za Mtwara “kwa kipindi kifupi kutokana na sababu za kibiashara wakati shirika likitathmini njia mbadala ya kuhudumia kituo hiki peke yake”.
“ATCL inawaomba radhi wateja wake kwa usumbufu utakaojitokeza kutokana na uamuzi huu,” ilisema zaidi taarifa ya Injinia Matindi kwani “usalama wa wateja ni kipaumbele cha ATCL.”
Source: Udaku Special