Kampuni ya ndege Tanzania (ATCL) inatarajia kuingiza nchini ndege zake mpya mbili mwishoni mwa mwezi ujao.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo ujio wa ndege hizo utaleta mapinduzi makubwa kihuduma na kiutendaji kwa kampuni hiyo.
Kaimu mkurugenzi mtendaji wa ATCL, Patrick Itule amesema ujio wa ndege hizo utairejeshea kampuni hiyo kwenye biashara ya ushindani dhidi ya kampuni nyingine za ndege hapa nchini.
Ndege hizo zinazotengenezwa na kampuni ya Bombardier ya nchini Canada zinatarajiwa kuingia nchini wiki ya tatu na ya nne ya Septemba, mwaka huu, zikipishana kwa wiki moja.
Mkurugenzi huyo amesisitiza kuwa ATCL haitakuwa tayari kuwavumilia wafanyakazi watakaoshindwa kuendana na kasi ya mabadiliko ya sasa.
Pia amesema ATCL tayari imeunda kikosi kazi kinachosimamia masuala mbalimbali, likiwemo la mafunzo ya watendaji wake mbalimbali ili kuendana na matakwa ya biashara hiyo kwa sasa.
Ndege hizo zina uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja na kwamba ujio wake utaongeza njia za kusafiri kwa kampuni hiyo kutoka njia mbili za sasa hadi kufikia njia zaidi ya kumi.