Askari Polisi namba H.3102 konstebo Bariki Michael (28), wa kituo cha Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa akikabiliwa na shtaka la kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 (jina limehifadhiwa).

Michael alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi, Erasto Phili na kusomewa shtaka linalomkabili na wakili wa serikali, Juma Maige.

Akisoma shtaka hilo, Maige alidai mshitakiwa alitenda kosa hilo Machi 14 2018 saa 4:00 asubuhi eneo la Kilimani mjini Ruangwa.

Wakili huyo alidai kuwa mshtakiwa, akiwa anatambua analofanya ni kosa, alipata mwanya wa kutekeleza tendo hilo nyumbani kwa mtoto huyo, ambaye pia ni jirani yake baada ya kubaki peke yake, ndipo akaitumia nafasi hiyo kumfuata na kumwingilia kwa nguvu.

Maige alidai kutokana na kitendo hicho, mlalamikaji alipiga kelele za kuomba msaada kutoka kwa majirani ambao walijitokeza na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo na kumpeleka kituo chao cha Polisi cha Ruangwa mjini.

Mshtakiwa alikana kosa na kupelekwa mahabusu baada ya kukosa dhamana na kesi yake imepangwa kutajwa mahakamani hapo April 12.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *