Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema na mkewe Neema Lema leo wanatarajiwa kupandishwa kizimbani kwa kosa la kumtukana mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Augustino Rwezile anatarajiwa kuwasomea hoja za awali washitakiwa hao.
Hoja hizo ilikuwa wasomewe Novemba 15, 2016 lakini zilikwama kusomwa kutokana na Lema kuugua ghafla na Wakili wa Serikali, Elizabeth Swai kumuomba hakimu kutumia busara ya Mahakama kuisogeza mbele kesi hiyo kutokana na hali ya mbunge huyo.
Kesi hiyo ya Lema na mkewe ya kumtumia ujumbe wa matusi Gambo, itaanza kusomwa maelezo ya awali ambayo nayo itakuwa tayari kwa kuanza kusikiliza baada ya upelelezi kukamilika.