Swansea City waliondoka kwenye eneo la hatari ya kushushwa daraja Ligi ya Premia kwa mara ya kwanza tangu Novemba baada ya kuwalaza Arsenal.
Kosa la ajabu kutoka kwa Petr Cech lilimpa nafasi Jordan Ayew kufunga bao na kuwaweka wenyeji kifua mbele kipindi cha pili kabla ya Sam Clucas kufunga bao lake la pili usiku wa Jumanne na kukamilisha ushindi wao wa 3-1.
Mesut Ozil alikuwa ametoa pasi safi na kumuwezesha Nacho Monreal kufunga bao la kwanza mechi hiyo dakika ya 33 kabla ya Clucas kuwasawazishia Swansea uwanjani Liberty Stadium dakika moja baadaye.
Vijana wa Arsene Wenger nao wameshinda mechi moja pekee kati ya 13 walizocheza ugenini msimu huu Ligi Kuu ya England.
Swansea wameonekana kuimarika sana chini ya meneja mpya Carlos Carvalhal ambapo wameshindwa mechi moja pekee kati ya nane walizocheza.
Ushindi wao dhidi ya Arsenal ndio wao wa pili mtawalia dhidi ya klabu iliyo nafasi sita za juu kwenye jedwali.
Liverpool ambao wamekuwa wakifunga mabao sana msimu huu walizimwa Liberty Stadium pia.