Aliyekuwa Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy anazuiliwa na polisi akihojiwa kuhusu tuhuma kwamba alipokea pesa za kufadhili kampeni zake kutoka kwa kiongozi wa zamani wa Libya Kanali Muammar Gaddafi.
Polisi wanachunguza tuhuma hizo kuhusiana na ufadhili wa fedha alizotumia kwenye kampeni za uchaguzi wa urais mwaka 2007.
Duru kutoka kwa mahakama zimesema rais huyo wa zamani alikuwa anahojiwa Nanterre, magharibi mwa Paris.
Mwaka 2013, Ufaransa ilianzisha uchunguzi kuhusu tuhuma kwamba kampeni ya Sarkozy ilipokea mchango kutoka kwa hazina ya pesa haramu za Gaddafi.
Duru zinasema mmoja wa mawaziri wa zamani wa Sarkozy na ambaye ni mshirika wake wa karibu Brice Hortefeux pia alihojiwa na polisi Jumanne.
Tuhuma hizo zilitolewa na mfanyabiashara Mfaransa mwenye asili ya Lebanon Ziad Takieddine na baadhi ya maafisa wa zamani wa Gaddafi.