Aliyekuwa mgombea ubunge wa viti maalum (Chadema) katika Jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro, Anitha Swai ameuawa na watu wasiojulikana.
Taarifa za awali zilizopatikana usiku wa kuamkia leo zimedai kuwa Anitha ambaye aligombea ubunge wa viti maalum mwaka 2015, alitekwa nyara wilayani Rombo na kuuawa maeneo ya TPC nje kidogo ya mji wa Moshi.
Vyanzo mbalimbali vya habari vimedokeza kuwa mara ya mwisho mwanasiasa huyo alionekana akiwa na watu wawili wilayani Rombo siku ya Jumatatu, Februari 27 na kuaga wanaelekea Arusha.
Hata hivyo, tangu siku hiyo Anitha hakuonekana hadi maiti yake ilipogunduliwa jana (Alhamisi) jioni maeneo ya TPC huku gari lake likiwa limetelekezwa maeneo ya Bomambuzi mjini Moshi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa amethibitisha kuokotwa kwa mwili huo, lakini amekataa kuthibitisha kama ni wa kada huyo wa Chadema.