Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi Felschemi Mramba amegeukia upande wa pili wa kumtumikia Mungu kwa kuhubiri injili.

 Mramba alikuwa mtumishi wa kwanza kuondolewa kwenye nafasi yake mwaka 2017, ambapo Januari mosi, Rais John Magufuli alitengua uteuzi wake kama Mtendaji Mkuu wa Tanesco na nafasi yake kuchukuliwa na Dk. Tito Mwinuka.

Utenguzi wa nafasi hiyo ulikuja siku chache baada ya Mramba kuwasilisha katika Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) maombi la kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 8.5, huku aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akitengua maombi hayo akieleza kuwa hakushirikishwa.

Kwa mujibu wa vipeperushi vilivyosambaa jana mtandaoni, Mramba anatarajia kutoa ‘neno la Injili’ kwenye semina maalum iliyoandaliwa, itakayofanyika Mei 30 hadi Juni 4, kwenye kanisa la waliookoka la Assemblies of God, Changanyikeni jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Mramba aliwaambia waandishi wa habari kuwa amekuwa akifundisha injili kwa muda mrefu lakini hakuwa na muda wa kutosha kutokana na majukumu, lakini sasa ana muda mzuri wa kufanya kazi hiyo.

Uongozi wa kanisa hilo pia ulithibisha kuwa Mramba atafundisha katika semina mbalimbali zinazoandaliwa jijini humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *