Mwili wa Boniface Pius, mkazi wa Chanika aliyefukiwa na kifusi katika machimbo ya Kigogo Fresh, umezikwa katika kifusi kilichomfukia baada ya juhudi za kuutoa mwili wake kukwama.
Pius alifukiwa na wenzake wanne wakati wakichimba udongo katika machimbo yasiyo rasmi, Alhamisi wiki hii.
Juzi, maiti moja ilitolewa kwenye kifusi hicho na jana aliokolewa mmoja akiwa hai, lakini miguu yake ilikuwa imekatika na mmoja aliyebaki ambaye ni Pius, ilishauriwa azikwe humo kutokana na mvua na hatari ya kifusi hicho kuwaangukia waokoaji.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema amesema udongo mwingi ulikuwa ukiporomoka wakati wa shughuli za uokoaji.
Watu hao waliangukiwa na kifusi siku ya Alhamisi wakiwa wanne na mmoja wao alikatika mguu, mwingine mwili wake ulipatikana siku hiyo hiyo na mwingine Rashid Fadhili yeye aliokolewa jana kabla ya kazi hiyo kufikia mwisho.
Pia amesema machimbo hayo yatafungwa na akatoa siku mbili watu wote kuondoa vitu vyao eneo hilo.
Kwa upande wa Baba mdogo wa marehemu, Pius, Aloyce Mlewa alizungumza kwa niaba ya familia kwamba wamekubaliana na ushauri wa mkuu wa wilaya wa kuzika mwili huo mahali hapo, kutokana na zoezi la uokoaji kuhatarisha usalama wa maisha ya wengine.