Wanamuziki wa Bongo Fleva, Alikiba na Diamond Platnumz ni miongoni mwa wasanii waliotajwa katika hatua za kuleta amani na kusambaza kiswahili nchini Congo.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Kikosi cha Wanajeshi cha Kulinda Amani Kongo kutoka Tanzania cha TANZBATT 7, DRC, Luteni Kanali John Ndunguru, Diamond na Kiba, wanastahili pongezi kwa kueneza Lugha ya Kiswahili ambayo hata wao imewarahisishia zoezi la kuleta amani nchini humo.
Kanali Ndunguru alisema waimbaji hao wa Tanzania wa muziki wa Kizazi Kipya na muziki wa Injili, wana mchango wao mkubwa.
Katika habari hiyo iliyorushwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa (UN), wanamuziki hao wamesaidia kwa kiasi kikubwa kuenea kwa Kiswahili katika nchi wanazolinda amani chini ya Umoja wa Mataifa.
Alizitaja nyimbo za Diamondi na Kiba kwa upande wa muziki wa Kizazi Kipya na waimbaji kama Rose Muhando na Christina Shusho kwa upande wa nyimbo za Injili.
Alisema nyimbo zao zimechangia kwa kiasi kikubwa kuenea kwa Lugha ya Kiswahili nchini Kongo, tofauti na lugha nyinginezo.