Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Alikiba amepata pigo baada ya kuthibitisha kuwa baadhi ya mipango yake imekwama kutokana na kifo cha mshirika wake wa karibu kibiashara ambaye alifariki kwa maambukizi ya ugonjwa wa Corona.
Kiba alifunguka hayo hivi karibuni akiwa nchini Kenya baada ya kuulizwa swali kuhusu ‘project’ yake ya kinywaji cha kuongeza nguvu cha Mo faya ambacho mwaka juzi alikizindua nchini humo.
Hata hivyo, kufuatia kudorora kwa mwendelezo wa matangazo ya kinywaji hicho, Kiba alifafanua kuwa kulijitokeza vikwazo mbalimbali katika biashara hiyo lakini kubwa ni suala la mshirika wake kufariki duniani. Alisema vikwazo vingine ilikuwa kubadilisha jina la kinywaji hicho ambalo taratibu zake zilileta changamoto.
“Lakini Corona ndio shida kweli kweli kwa sababu mmoja wa ma-patner wangu alipata Corona na kufariki ilibidi tutulie kidogo, haya mengine yapo chini ya kapeti lakini ni kweli nilikuja hadi Kenya kufanya uzinduzi.
“Ila tupo katika hatua ya mwisho kukamilisha hilo suala, pia kuna bidhaa ambayo tutaiweka kwenye soko muda si mrefu,” alisema Kiba.
Pamoja na mambo mengine alisema si kweli kwamba ni mbinafsi kutokana na msimamo wake wa kutowa-follow watu kwenye akaunti yake ya Instagram ambayo hadi sasa ina wafuasi milioni 6.9 huku yeye akiwa amem-follow Rais Samia Hassan Suluhu pekee.
Kiba alisema yuko tofauti lakini si kwa ubaya, hivyo amejiwekea msimamo kutathmini ni watu gani wanaweza kufuatilia mziki wake hata kama yeye hajawafuata kwenye mtandao huo.
Alisema kwa kuwa sasa ameona akaunti yake inakua, hana haja ya kuwafuata kwani sasa ametambua kuwa anao mashabiki wa kweli wanaounga mkono muziki wake.