Mwanamuziki wa hip hop nchini, Stamina amefunguka na kusema kuwa amesikitishwa na Naibu Waziri wa Sanaa na Utamaduni kumfungia mwanamuziki mwenzake Roma asihusishe na muziki kwa miezi sita.
Stamina amesema kuwa ameshangazwa na maamuzi yaliyofanywa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza kwa hatua hiyo aliyochukua.
Stamina amefunguka hayo baada ya kusikia Roma amefungiwa kujihusisha na sanaa kisa kutofanya marekebisho ya wimbo wao wa Kibamia.
Pia Stamina amesema kuwa awali walipoongea na Naibu Waziri huyo aliwapa miezi sita ya kufanya marekebisho ya wimbo huo sasa iweje amechukua maamuzi ili hali hata muda ambao walipewa haujakwisha.
Stamina na Roma Mkatoliki kwa pamoja wanaunda kundi la ROSTAM ambao ndio wamiliki wa wimbo huo wa Kibamia lakini matokeo yake Roma Mkatoliki amechukuliwa adhabu peke yake kwa wimbo wa kundi hilo.