Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kuwa hakuna mtu yoyote hatakayemnyamazisha katika mapambano ya vita ya dawa za kulevya.
Makonda ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa anazungumza na wadau na waathirika wa dawa za kulevya kuhusu mikakati yake baada ya kufikisha mwaka mmoja akiongoza mkoa wa Dar es Salaam.
Mkuu wa mkoa huyo amesema kumekuwa na maneno mengi yakizungumzwa, baada ya kuanza kwa sakata la dawa kulevya, jambo ambalo linaashiria vita hiyo imewagusa wengi.
Pia ameongeza kuwa wapo watu waliobeza mbinu aliyoitumia katika kuwataja wafanyabiashara, watumiaji na waingizaji wa dawa hizo, lakini akasema kama wangeamua kufanya bila kuwataja, wananchi wengi wangeendelea kuangamia.
Makonda amesema kuwa kuwa mpaka sasa wapo vijana zaidi ya 11,000 ambao wapo tayari kuachana na matumizi ya dawa za kulevya.
Kwa upande mwingine Makonda amesema ofisi yake wakishirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango, wataanzisha operesheni ya kuyapitia maduka ya kubadilishia fedha ili kujiridhisha kama yanatumika katika kutakatisha fedha za wauza dawa za kulevya.