Mwanaharakati aliyeshiriki kupigana dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, Ahmed Kathrada amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 87.

Kathrada amefariki dunia akiwa katika hospitali moja mjini Johannesburg baada ya kuugua kwa muda mfupi, kufuatia upasuaji aliofanyiwa kwenye ubongo wake.

Pamoja na Nelson Mandela, Bw Kathrada alikuwa miongoni mwa wanaharakati wanane wa African National Congress waliohukumiwa kufungwa jela maisha mwaka 1964.

Kathrada alikaa jela miaka 26 katika gereza hatari la Robben Island na aliachiliwa huru mwaka 1989.

Rais Mandela baadaye alimshawishi kujiunga na serikali ya Afrika Kusini baada ya kutoka jela nchini humo.

Ahmed Kathrada aliondoka bungeni 1999, lakini aliendelea kushiriki katika siasa nchini Afrika Kusini.

Kiongozi huyo alikosoa mwelekeo wa chama cha ANC hivi majuzi na kumtaka Rais Jacob Zuma kujiuzulu kutokana na matumizi mabaya ya madaraka .

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *