Mkoa wa Dar es Salaam unatarajia kujenga vituo vikubwa vya Polisi 20 ili kuimarisha ulinzi, pamoja na kuondoa changamoto ya ubovu wa vituo kwa vilivyopo ambayo imegeuka kero kwa askari na wananchi wa mkoa huo wanaovitumia.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda wakati alipofanya ziara katika vituo vidogo vya Polisi vilivyopo katika mkoa huo.
Makonda alisema vituo vyote vinatarajia kutumia Sh bilioni 10 hadi kukamilika na kila kimoja kitakuwa na uwezo wa kuwa na askari 100.
Amesema uwepo wa vituo hivyo utasaidia kuondoa changamoto ya wizi wa silaha zilizokuwa zikuibwa na majambazi waliokuwa wakivamia vituo na kuwaua askari.
Pia mkuu wa mkoa Makonda ametoa mwito kwa wananchi kushirikiana kuwafichua wezi wanaotumia pikipiki, majambazi na wauza dawa za kulevya ili wachukuliwe hatua za kisheria na Dar es Salaam ibaki kuwa safi.