Watahiniwa 408,442 wamesajiliwa na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne unaotarajia kuanza leo hadi Novemba 18, mwaka huu.

Akizungumzia maandalizi ya mtihani huo, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde amesema kati ya watahiniwa waliosajiliwa wa shule ni 355,995 na wa kujitegemea ni 52,447.

Mwaka 2015, waliosajiliwa kufanya mtihani ni 448,382, hivyo kuwapo na upungufu wa watahiniwa 39,940.

Dk Msonde amesema kati ya watahiniwa wa shule 355,447 waliosajiliwa, wavulana ni 173,423 ambao ni asilimia 48.72 na wasichana ni 182,572 sawa na asilimia 51.28. Watahiniwa 59 ni wasioona na wenye uoni hafifu ni 283.

Amesema kati ya watahiniwa wa kujitegemea 52,447 waliosajiliwa, wanaume ni 25,529 sawa na asilimia 48.68 na wanawake ni 26,918 sawa na asilimia 51.32.

Pia watahiniwa wa kujitegemea wasioona wako saba, wanawake watatu na wanaume ni wanne. Mwaka jana watahiniwa wa kujitegemea walikuwa ni 54,317.

Kuhusu watahiniwa waliosajiliwa kufanya Mtihani wa Maarifa (QT), Dk Msonde alisema baraza limesajili 20,634 ambao wanaume ni 7,819 sawa na asilimia 37.89 na wanawake ni 12,815 sawa na asilimia 62.11. Mwaka jana, idadi ya watahiniwa wa QT walikuwa 19,547.

Aidha, baraza limewaasa wanafunzi, walimu kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu wa mtihani kwani watakaobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kufutiwa matokeo yote.

Katika matokeo ya darasa la saba yaliyotangazwa wiki iliyopita, wanafunzi 238 kutoka shule sita walifutiwa matokeo yao yote kutokana na udanganyifu wa mtihani.

Dk Msonde alizitaka Kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri, kuhakikisha kuwa taratibu zote za uendeshaji mitihani ya Taifa zinazingatiwa ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa mazingira ya vituo yapo salama, tulivu na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha udanganyifu. Pia Dk Msonde alitoa mwito kwa wasimamizi wote kufanya kazi yao kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *