Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema itawapokonya mikopo baadhi ya wanafunzi ambao uhakiki utawabaini kuwa hawakuwa wanastahili kupewa mikopo waliyokopeshwa.

Utaratibu huo utawagusa wanafunzi wapya na wale wanaoendelea na masomo baada ya bodi kufanya uhakiki na uchunguzi wa taarifa za wanufaika wote wa mikopo. Uchunguzi huo unaanza kesho.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul Razaq Badru amema wanafunzi watakaokutwa na hadhi zisizostahili wataondokewa na sifa za kuendelea kupata mikopo na kulazimika kurejesha kiasi cha fedha watakachokuwa wamepokea tayari.

Amefafanua kuwa kiasi cha fedha ambacho watalazimika kurejesha wanafunzi ambao watakutwa hawana uhitaji ni fedha walizochukua kuanzia Novemba mwaka huu.

Uamuzi huo wa bodi wa kutangaza kuwapoka mikopo baadhi ya wanafunzi ni wa kwanza kufanywa na chombo hicho ambacho mara kwa mara kimekuwa kinatoa mikopo kwa kufuata sera za serikali.

Miaka ya nyuma wanufaika wa mikopo hiyo walikuwa ni wanafunzi wenye ufaulu wa daraja la kwanza na la pili bila kujali familia wanazotoka. Lakini mwaka huu, serikali imetangaza kuwa sera ya mikopo kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya vipaumbele vya taifa na uyatima, ulemavu, ualimu wa sayansi na hisabati, sayansi ya tiba na afya, sayansi asilia, sayansi ya ardhi, usanifu majengo na miundombinu na uhandisi wa viwanda, kilimo, mifugo na gesi asilia na mabadiliko ya tabianchi.

Badru katika maelezo yake amefafanua kuwa katika kuhakikisha wanafunzi wote wanahakikiwa, bodi hiyo imeandaa dodoso ambalo litawekwa kwenye tovuti ya bodi hiyo na wanafunzi wote ambao wananufaika na mkopo wa bodi ni lazima wajaze taarifa za kiuchumi za wazazi na walezi wao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *