Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva ameitaka serikali kubadili muundo wa tume hiyo ili iwe na ofisi na watumishi katika kila halmashauri nchini na ofisi ya Zanzibar.
Amesema hatua hiyo itawezesha NEC kufanya kazi zake kwa uhuru zaidi, badala ya kutegemea wakurugenzi wa halmashauri (Ma-DED).
Tathimini hiyo imetolewa ikiwa ni mwaka mmoja tangu Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli kutangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi huo.
Lubuva amesema serikali ifanyie mapitio ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 na Sheria ya Serikali za Mitaa Sura 292 ili kurekebisha vifungu vinavyokinzana.
Amesema baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, tume iliamua kufanya tathimini kwa lengo la kupata mrejesho juu ya utekelezaji wa Uchaguzi Mkuu kutoka kwa wadau. Alisema ni mara ya kwanza kwa tume kufanya tathimini tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993.
Amesema changamoto zilizojitokeza kwa mujibu wa wadau waliohojiwa ni pamoja na mpiga kura kutoruhusiwa kupiga kura katika eneo tofauti na lile alilojiandikisha.
Pia wapiga kura kushindwa kupiga kura siku ya uchaguzi kutokana na kugawa mipaka ya kiutawala na majimbo ya uchaguzi, baada ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura na muda mfupi uliotolewa kujiandikisha na uwekaji wazi wa daftari la awali la wapiga kura.
Amesema tathimini inaonesha katika baadhi ya maeneo, watu waliojitokeza kupiga kura ni wachache, ukilinganisha na idadi ya wapiga kura waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.