Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imefanya operesheni ya ukaguzi wa dawa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini na kufanikiwa kukamata dawa bandia za aina tano katika maghala na maduka mbalimbali ya dawa.
Aidha maduka 17 yaliyokutwa na dawa bandia na za serikali yamefungwa na dawa zote zilizokuwa na makosa zimekamatwa.
Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo amesema dawa hizo bandia zipo kwenye makundi mawili ambazo ni dawa za malaria na dawa za viua vijisumu (antibiotics).
Amesema ukaguzi huo ulifanyika kufuatia taarifa za awali za uwepo wa dawa bandia katika maeneo ya mikoa ya Geita na Mara katika kipindi cha Agosti na Septemba, 2016.
Amesema operesheni ya ukaguzi huo ulifanywa na wataalamu wa TFDA kwa kushirikisha maofisa kutoka Baraza la Famasi, Jeshi la Polisi, ofisi za waganga wakuu wa mikoa na halmashauri za wilaya husika.
Aliyataja maeneo yaliyohusika na ukaguzi huo kuwa ni pamoja na famasi, maghala ya dawa, zahanati, maduka ya dawa za mifugo pamoja na maduka ya dawa muhimu.