Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inakusudia kuimarisha elimu ya msingi na mjumuisho ili kuona malengo ya kujua kusoma na kuandika kwa wanafunzi yanafikiwa katika hatua za awali.
Aidha, katika kufanikisha hilo, serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo imetenga Sh bilioni tatu.
Hayo yalisemwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Abdallah Mzee wakati alipozungumza mara baada ya kumalizika kwa mkutano uliowashirikisha wadau katika sekta ya elimu nchini.
Amesema SMZ imeifanya elimu ya msingi kuwa ya lazima ambapo kazi kubwa inayofanywa kwa sasa ni kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa kuona inawafikia walengwa katika ubora unaotakiwa.
Ameongeza kuwa, katika kuimarisha elimu ya mjumuisho, Wizara imeweka kipaumbele cha upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wakiwemo walemavu.
Amesema Wizara ya Elimu imetenga baadhi ya shule ambazo zitakuwa zikitoa elimu ya mjumuisho kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu huku walimu wanaotoa elimu hiyo wakipewa mbinu za kufundisha.
Serikali ya Zanzibar imetangaza elimu ya msingi na maandalizi kuwa ya lazima ambapo kazi kubwa inayofanywa kwa sasa ni kuboresha elimu inayotolewa kwa wanafunzi pamoja na ufaulu wake.