Waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ametakiwa kuendeleza mashamba yake mawili ndani ya siku 90 la sivyo Serikali itafuta hati ya umiliki wake.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema hati ya mashamba ya Sumaye iko katika hatua ya kufutwa na kwamba Afisa Ardhi mteule wa wilaya ya Kinondoni, Rehema Mwinuka ameshatoa barua ya notisi.
Sumaye anamiliki mashamba hayo mawili moja likiwa mkoani Morogoro na lingine likiwa eneo la Mwabepande nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Kwa upande wake Sumaye amesema kuwa notisi hiyo ni matokeo ya chuki ya Serikali dhidi yake baada ya kuhama CCM na kujiunga na CHADEMA.
Sumaye alikuwa msemaji tegemeo kwenye mikutano ya kampeni za UKAWA katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.