Wazanzibari 40,000 wamefungua kesi mahakamani kupinga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kesi hiyo imefunguliwa katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) na Rashid Salum Adiy kwa niaba ya wenzake 39,999, katika Masijala ndogo ya mahakama hiyo iliyoko jijini Dar es Salaam.

Wadaiwa katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Adiy amesema kuwa msingi wa kesi hiyo ni kwamba Muungano huo haukuanzishwa kisheria.

Amesema kutokana na nyaraka walizonazo wanapinga hati ya Muungano inayodaiwa ilisainiwa Aprili 22, 1964 na wanapinga uamuzi wa Baraza la Mapinduzi kuridhia Muungano huo.

Katika kesi hiyo wanapinga barua ya Mei 6, 1964, iliyopelekwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), kuelezea kutambuliwa kwa Muungano huo.

Pia wanapinga uhalali wa barua ya Novemba 2, 1964 iliyopelekwa UN ikielezea matumizi ya jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria iliyopitishwa na Bunge Desemba 10, 1964 ikielezea matumizi ya jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Adiy na wenzake wanadai kwa kuwa Muungano ni wa kisiasa, ndiyo maana hauwezi kuleta manufaa kwa pande zote mbili hususani uwiano wa kiuchumi na kielimu.

Baada ya kuwasilisha nyaraka zao wanasubiri kesi hiyo isajiliwe kwa kupewa namba katika Mahakama hiyo na kupangiwa taratibu za usikilizwaji wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *