Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema serikali itaendelea kudumisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria  kati ya Tanzania na India.

Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo leo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa India nchini Sandeep Arya Ikulu jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais amesema mahusiano kati ya Tanzania na India yamesaidia kunufaisha wananchi wa nchi mbili hasa katika masuala ya kibiashara,miradi ya maendeleo na hivyo mahusiano hayo ni muhimu yakaendelezwa na kudumishwa.

 

Pia Makamu wa Rais ameiomba serikali ya India kuisaidia Tanzania katika mpango utakaosaidia wakulima kupata taarifa mbalimbali zinazohusu kilimo na masoko ya bidhaa zao kupitia simu za mkononi ili kuondoa usumbufu mkubwa wanaopata wakulima kwa sasa hasa kuhusu masoko.

 

Kwa upande wake, Balozi wa India nchini Tanzania Sandeep Arya amemhakikishia Makamu wa Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan serikali yake itakuwa bega kwa bega na Tanzania katika kuhakikisha wananchi wa pande Mbili wananufaika na mahusiano yaliyopo.

 

Balozi Sandeep Arya amesisitiza kuwa serikali ya India itaendelea kuisaidia Tanzania katika uimarishaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na miradi ya maendeleo na uimarishaji wa shughuli za kiuchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *