CHADEMA wamesema wapo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kufungua kesi kulalamikia uchaguzi wa umeya uliofanyika katika Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene amesema kuwa maandalizi yanaendelea kufanyika, kuhakikisha wanafungua kesi, kwani wanaamini sheria na kanuni hazikufuatwa katika uchaguzi huo uliofanyika juzi.
Benjamin Sitta ameshinda kwenye uchaguzi huo na kuwa Meya wa Kinondoni na Naibu wake alichaguliwa Jumanne Mbunju, wote kutoka CCM.
Kwa upande wa Ubungo, ambako madiwani wa upande wa Chadema pamoja na wajumbe wengine waliostahili kupiga kura kumchagua Meya na Naibu wake waligomea kufanyika uchaguzi, wakidai kuwepo na mapungufu kadhaa ikiwa ni pamoja na taarifa wajumbe kuzipata muda mfupi kabla ya uchaguzi, Makene alidai bado msimamo wao ni ule ule.
Amesema wajumbe wa upande wa Chadema hawatapiga kura mpaka pale sheria na kanuni zinazoendesha uchaguzi huo zifuatwe.