Serikali kuwekeza na kutekeleza sera na mipango ya kupunguza tatizo la maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi na vifo vya uzazi hususani kwa vijana wa kike ambao ndio wamebainika kuwa sehemu kubwa ya watu wanaopata maambukizi ya ugonjwa huo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangallah amesema kuwa watu wazima wamekuwa na mtindo wa kuanzisha uhusiano na mabinti wadogo, hali inayochangia vijana hao kuusambaza ugonjwa huo kwa vijana wenzao, hivyo kuongeza kasi ya maambukizi.
Dk Kigwangallah aliyasema hayo mjini Dodoma wakati akizungumza kwenye semina ya siku mbili ya wabunge kuhusu matatizo ya maambukizi ya Ukimwi, vifo vya uzazi na mimba za utotoni iliyoandaliwa na Mabunge ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika ( SADC) na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids).
Amesema kwa tathmini iliyofanywa imebainika kuwa watu wazima wengi ambao tayari wana wenza wao, hupenda kuanzisha uhusiano na vibinti vidogo ambao nao wana wenza wao na matokeo yake ugonjwa huo husambazwa kwa kasi kupitia mzunguko huo.