Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema hadi kufikia mwaka 2025, sekta ya madini nchini inapaswa ichangie asilimia 10 kwenye Pato la Taifa.

Katika kipindi cha mwaka 2015 sekta hiyo imechangia asilimia 4.3 kutoka asilimia 3.7 kwa mwaka 2014, kiasi ambacho waziri huyo amesema bado ni kidogo.

Muhongo aliyasema hayo mjini Dodoma mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakati akitoa taarifa kuhusu shughuli za utafutaji madini na maendeleo ya sekta ya madini.

Waziri huyo ametaja changamoto zinazoifanya sekta hiyo kuwa na mchango mdogo katika Pato la Taifa kuwa ni pamoja na kushuka kwa bei ya madini kwenye soko la dunia na kutokuanzishwa kwa migodi mingine mikubwa ya uchimbaji hivi karibuni.

Amesema kwa sasa uwezo wa uzalishaji wa dhahabu kwa migodi yote nchini ni wakia milioni 1.25 kwa mwaka na uzalishaji kuanzia mwaka 2011 hadi 2015 ni wakia milioni 5.68 sawa na tani 176.7 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 9.06 sawa na Sh trilioni 19.7.

Waziri huyo amefafanua kuwa ipo mipango mbalimbali ya kuendeleza shughuli za madini nchini ikiwemo kuboresha ukusanyaji na usambazaji wa taarifa na takwimu za kijiosayansi, udhibiti wa utoroshwaji wa madini na ukaguzi katika shughuli za uzalishaji madini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *