Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amesema kuwa Rais Magufuli amemuhakikishia kuwa yeye ndiyo mkuu wa mkoa wa Arusha.
Hatua hiyo inakuwaja baada ya kuenea kwa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Rais Magufuli amemuengua ukuu wa mkoa wa Arusha kitu ambacho si kweli.
Gambo amesema hayo wakati akitoa maelezo ya mwisho katika kikao cha wafanyabiashara wakubwa wa mkoani Arusha, aliokutana nao kusikiliza changamoto, zinazowakabili na kuzifanyia kazi ili waweze kufanya kazi bila wasiwasi.
Mkuu wa mkoa huyo amewaeleza wafanyabiashara hao kuwa Rais amempigia simu na kumhakikishia kuwa yeye ndiye Mkuu wa Mkoa wa Arusha na hakuna mabadiliko yoyote kwa sasa.
Gambo amesema baada ya kuzungumza kwa simu na Rais, Rais aliomba kuongea na kiongozi wa chama cha wafanyabiashara wa Mkoa wa Arusha na akamkabidhi simu Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoani Arusha, Wolter Maeda.
Maeda amekiri kuongea na Rais Magufuli na kusema kuwa Rais amemwambia kuwa Arusha, inatakiwa kuwa ya amani na utulivu na aliwaasa kufanya biashara bila ya wasiwasi na kulipa kodi inayostahili.
Pia amesema kuwa wafanyabiashara, wasiogope chochote na iwapo watendaji wa serikali yake, watakuwa wakifanya kazi kwa vitisho, wanapaswa kutoa taarifa mara moja kwa viongozi wa juu wa mkoa, kwani wanapaswa kulipa kodi inayostahili kwa mujibu wa sheria.
Gambo amewataka wafanyabiashara Arusha, kushirikiana na kufanya kazi kwa malengo ya kukuza uchumi wa Mkoa wa Arusha na sio vinginevyo na aliwaahidi kutoa ushirikiano wa hali na mali.