Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amesikitishwa na kitendo cha kutoelewana kati ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo na Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Godbless Lema.
Zitto kupitia ukurasa wake wa facebook amesema anakasirishwa sana kuona viongozi wanafanya mambo ya hovyo jambo ambalo litafanya vijana washindwe kuaminiwa katika nafasi wanazopewa kwa kutotumia hekima na busara katika majukumu yao.
Zitto amemtaka Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema kupunguza munkari katika majukumu yake kwani mchango wake kwa wananchi wa Arusha hauwezi kufutika kirahisi.
Pamoja na hayo Zitto amewashauri viongozi hao kukaa pamoja meza moja na kujenga Arusha na kuacha kuonesha hasira zao hadharani kwa wananchi.
Kauli ya Zitto imefuatia kutokuwepo kwa maelewano ya mara kwa mara baina ya viongozi hao ikiwemo tukio la jana la Mbunge Lema kutofautiana na Mkuu wa Mkoa Mrisho Gambo hadharani wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali.