Mkurugenzi wa Idara ya Petroli wa Ewura, Godwin Samweli amesema kuwa mamlaka hiyo itaanza kutoa bei kikomo kwa gesi ya kupikia inayotokana na zao la mafuta ya petroli, utaratibu unaotarajia kuanza Januari mwakani.
Mbali na kuelezwa majukumu ya Ewura katika kudhibiti biashara ya mafuta nchini, wafanyabiashara hao walifundishwa jinsi sheria na kanuni zinavyofanya kazi katika udhibiti wa sekta ya petroli nchini.
Akifafanua kuhusu udhibiti wa bei ya gesi ya kupikia, Samweli amesema baada ya Ewura kufanya mkutano na wadau wa sekta hiyo, baadaye mwaka huu itakamilisha kanuni ya kupanga bei zitakazoanza kutumika mapema mwakani. Alisema mpango huo utatekelezwa baada ya Ewura kutengeneza utaratibu, utakaoufanya Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kuanza kuingiza gesi ya kupikia kwa wingi.
Wakati huo huo, Ewura imewataka wauzaji wote wa gesi ya kupikia kuwa na mizani ya kupimia gesi wanayouza kama sheria inavyotaka, vinginevyo watalazimika kulipa faini ya Sh milioni tatu hadi Sh milioni tano au kunyang’anywa leseni endapo watakutwa na kosa hilo. Samweli alisema pia ni makosa kisheria, kufanya biashara ya gesi ya kupikia bila kuwa na leseni ya Ewura.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi amesema mamlaka hiyo ina wajibu wa kudhibiti huduma za nishati (umeme, petroli na gesi asilia), maji na usafi wa mazingira, kwa kutumia mfumo shirikishi unaowashirikisha wadau wote kabla ya kufanya maamuzi ya kiudhibiti.