Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe.Qian Keming.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamekubaliana kuharakisha miradi inayotekelezwa kwa ushirikiano wa nchi hizo mbili ukiwemo mradi wa ujenzi wa reli ya kati.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam Rais Magufuli amemueleza Mhe. Qian Keming kuwa Serikali yake ya awamu ya tano inataka kuona mambo yakifanyika na kutoa matokeo bila kupoteza muda na kwamba angependa wadau wa maendeleo hasa nchi ya China ambayo ni ndugu na rafiki mkubwa wa Tanzania iende katika kasi hiyo hiyo.
Rais Magufuli ameuzungumzia mradi wa ujenzi wa reli ya kati ya kutoka Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma na kuunganisha nchi za Rwanda na Burundi ambao Tanzania imetenga Shilingi Trilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi katika bajeti hii, kwa kutaka China ambayo imekubali kushiriki katika ujenzi iendane na kasi ya Serikali yake.
Dkt. Magufuli ameongeza kuwa mradi huo una manufaa makubwa kwa Tanzania na nchi nyingine nane zinazotegemea bandari ya Dar es Salaam na kwamba kukamilika kwake kutatoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania ambayo imedharia kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Biashara wa China Mheshimiwa Qian Keming amempongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya ya kukuza uchumi wa Tanzania, kupiga vita rushwa na kwa namna ya kipekee kwa dhamira yake ya kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano na China na ameahidi kuwa Serikali ya China itaongeza msukumo katika uharakishaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa reli ya kati.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Dkt. Lu Youqing, Makamu wa Rais wa Benki ya Exim ya China Bw. Sun Ping, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles John Mwijage na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango.