Mkuu wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Glorius Luoga amewaagiza polisi kuwakamata Ofisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Mji Tarime, George Ogutu na Mkuu wa Shule ya Sekondari Tarime, Marwa Matiko kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha Sh 21,052,500.

Fedha hizo ni kati ya Sh 29,969,000 walizopokea kwa ajili ya fidia ya ada ya elimu bila malipo huku wakiwa na majina ya wanafunzi 577 ambao wanadaiwa kuwa wengi ni wanafunzi hewa badala ya wanafunzi halali 176.

Ametoa agizo hilo jana wakati wa kikao alichofanya ghafla katika shule hiyo ya sekondari Tarime akiongozana na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama Wilaya.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuanzia Januari mwaka huu hadi Septemba, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kupitia elimu bila malipo ilituma kwa shule hiyo ya sekondari jumla ya Sh 29,969,000 kwa ajili ya kuwahudumia wanafunzi.

Kwea mujibu wa Luoga, kila mwanafunzi hutumiwa ada ya Sh 70,000 kila mwezi na katika shule hiyo kuna wanafunzi halali 176 wa elimu ya juu ambao walitakiwa kutumia Sh 9,239,999.99 katika kipindi hicho cha miezi tisa.

Watuhumiwa hao George na Marwa walijaribu kujitetea kuwa fedha hizo walizipokea bila maelezo ya ufafanuzi wa matumizi yakiwemo ya ada za wanafunzi elimu bila malipo, ruzuku maalumu na fedha za chakula, lakini Mkuu wa Wilaya alipingana na maelezo yao huku akisema hawawezi kupokea fedha hizo tangu Januari hadi Septemba miezi tisa bila kuelewa ufafanuzi wake huku wakijua kuna wanafunzi hewa walioandikishwa kutoka 176 hadi 577 na kusema huu ni wizi mkubwa kwa mali ya umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *