Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amesema kuwa vifaa vya maabara za shule za sekondari vyenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 12 vinatarajia kuwasili nchini mwishoni mwa mwezi ujao.
Profesa Ndalichako amesema zipo kontena takribani 30 za vifaa vya maabara vilivyonunuliwa na serikali kutoka nchi za Urusi na Uingereza ambavyo baada ya kuwasili vitasambazwa katika shule za sekondari hasa senye maabara zilizojengwa na wananchi.
Amesema lengo la serikali ni kuona maabara zinaanza kufanya kazi Januari mwakani baada ya shule kufunguliwa na wanafunzi kuanza muhula wa masomo.
Amebainisha kuwa maabara nyingi tangu wananchi wakamilishe ujenzi wake zimebaki magofu kwa kuwa haziwezi kutumika kutokana na kukosekana kwa vifaa na ndiyo sababu serikali imechukua juhudi za makusudi kununua vifaa hivyo.
Pia alisisitiza kuwa usambazaji wa vifaa utazingatia vigezo muhimu na ndiyo sababu vitagawiwa kwenye shule za sekondari zilizokamilisha ujenzi na hiyo itafanyika baada ya uhakiki.