Mbeya City imetoa onyo kwa Simba kuwa hawatatoka salama kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kesho, kwani wamejipanga kuifunga na kubakiza pointi tatu.
Msemaji wa Mbeya City, Dismas Ten amesema kuwa Simba isitegemee kushinda kwa urahisi kama ilivyofanya katika mechi zake zilizopita kwani hata wao wamejipanga na wanahitaji ushindi.
Amesema wanaifahamu ni timu nzuri na wanawaheshimu, lakini ubora wao hauwaogopeshi katika kujituma na kupata ushindi.
Ten amesema kinachohitajika ni waamuzi wachezeshe mchezo kwa kufuata sheria 17, ili mashabiki wapate burudani na kufurahia ushindi kwa timu yao.
Timu hiyo inajivunia kufikisha pointi 12 katika michezo minane iliyocheza hadi sasa ikishika nafasi ya nne, kwenye msimamo wa ligi.
Kwa upande wa Simba, huo utakuwa ni mchezo wake wa kwanza nje ya mkoa wake, ikitarajiwa kuendelea ushindi walioanza nao tangu kuanza kwa msimu na kutesa kileleni kwa pointi 17 katika michezo saba iliyocheza.
Msemaji huyo wa Mbeya City alisema wachezaji wake waliokuwa majeruhi Haruna Shamte na Sankhani Mkandawile wameanza mazoezi tayari kuivaa Simba kesho.