Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli ametaka utekelezaji wa diplomasia ya uchumi utiliwe mkazo katika uwekezaji kwenye sekta ya viwanda.

Rais aliyasema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam juzi jioni alipokutana na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani.

Mkutano huo uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, ulihudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Rais Magufuli aliyehutubia na kuongoza majadiliano juu ya masuala mbalimbali ya shughuli za mabalozi, alisema Tanzania imeweka dhamira ya kuikuza sekta ya viwanda kutoka ukuaji wa asilimia 7.3 hadi kufikia asilimia 15 ifikapo mwaka 2021 na kuzalisha ajira kwa asilimia 40.

Maeneo mengine ambayo Rais alitaka Mabalozi wayafanyie kazi ni kutangaza na kuwavutia watalii kuja nchini, kufanyia kazi fursa zote zenye manufaa kwa Tanzania katika nchi wanakowakilisha, kulinda mali za nchi zilizopo katika nchi hizo na kufuatilia utekelezaji wa mikataba ya biashara na uwekezaji inayofanywa kati ya Tanzania na nchi wanakowakilisha.

Aliwataka Mabalozi wote kufanya kazi kwa juhudi, kuondoa kasoro za utendaji kazi ambazo zimekuwa zikilalamikiwa katika ofisi zao na kubana matumizi ya fedha yasiyokuwa ya lazima.

Rais pia aliitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kujipanga na kudhibiti mianya yote ya matumizi mabaya ya fedha za umma ambazo zimekuwa zikitumika katika safari za nje ya nchi na matumizi mengine yasiyo ya lazima.

Aliwaagiza kuhakikisha watumishi wote ambao wapo katika ofisi za ubalozi kwenye nchi mbalimbali bila sababu za msingi wanarejeshwa nchini ili kupunguza mzigo wa gharama kwa Serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *