Makamo wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amezindua nembo ya Fahari ya Tanzania pamoja na kutoa tuzo kwa kampuni 50 za hapa nchini zinazofanya vyema katika biashara.
Tuzo hiyo imeandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania ( TanTrade) Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) pamoja na GS1. Samia alizindua nembo hiyo juzi katika Ukumbi wa Mlimani City, hafla ambayo ilihudhuriwa na wafanyabiashara mbalimbali nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Samia alisema kuwa serikali itahakikisha kuwa inaendelea kuimarisha mazingira kwa wafanyabiashara wa Tanzania ili waweze kuuza bidhaa zao nje ya nchi.
Amesema kuwa hiyo itaenda sambamba na kulinda bidhaa zinazozalishwa hapa nchini dhidi ya ushindani wa bidhaa za nje ya nchi na kuongeza kuwa lengo ni kuziuza bidhaa za hapa nchini kwenda kwenye nchi hizo za nje.
Kampuni ambazo zilitunukiwa tuzo hizo ziligawanywa kwenye makundi mbalimbali ambapo katika kundi la Vifaa vya Ujenzi, Kampuni Bora ya Saruji ni Twiga Cement, ya Rangi ni Gold Star, Nyaya ni Africa, Kiboko iliibuka kuwa ni Kampuni Bora ya Matangi ya Maji, Uezekaji ni Simba Dumu.
Tuzo ya Wasindikaji Bora wa Chakula ilienda kwa Tanga Fresh kama Kampuni Bora ya Maziwa, Unga ilienda kwa Azam Sembe, Ngano ilienda kwa Azam Wheat Flour, Sandro iliibuka Kampuni Bora ya Mafuta ya Kula, Chai Bora iliibuka na Tuzo katika Majani ya Chai.
Katika Kahawa iliyoshinda ni Africafe, Sukari Tuzo ilienda kwa Bwana Sukari, Mikate ilienda kwa Super Loaf huku Red Gold ikishinda Tuzo ya Kampuni Bora ya Bidhaa za Nyanya.
Kwa upande wa Vinywaji iliyoshinda ni Bia ya Kilimanjaro, huku Vinywaji Vikali ikishinda Konyagi, Mvinyo ilishinda Dodoma Wine, Maji ya kunywa imeshinda Maji ya Kilimanjaro, Juisi imeshinda Azam Embe na Vinywaji vya Kuongeza Nguvu imeshinda Grand Malt.
Katika tuzo ya Bidhaa za Nyumbani washindi ni Cello, Magodoro Dodoma, Rexal, Kioo huku katika Chakula imeshinda Alaska Rice katika tuzo nyingine Dawa ya Meno ya Whitedent ilishinda, Sabuni ya Mche ya Mshindi ilishinda pia huku Sabuni ya Family ilishinda pia, na Mafuta ya Kujipaka ya Baby Care pamoja na Dawa ya Mbu ya Expel.