Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imezifuta shule nyingine za awali na msingi nchini ambazo hazijasajiliwa zaidi ya 10 kuanzia Desemba mwaka jana.

Shule tano kati ya 40 zilizokuwa zimefutiwa usajili zimekamilisha taratibu na kurejeshewa usajili wake.

Kaimu Mkurugenzi wa Usajili wa Shule katika wizara hiyo, Khadija Mcheka amesema mpaka sasa bado wanaendelea na ukaguzi kubaini shule ambazo hazijasajiliwa.

Alizitaja shule ambazo zimefutwa kwa kutosajiliwa kuwa ni Mwandai Junior Academy, shule ya msingi DACETE, shule za msingi Malaika na Fares Kisingo (FK) za wilaya ya Kinondoni. Nyingine ni shule ya msingi The Unity, shule ya sekondari Jotac iliyopo eneo la Kipunguni, Verena iliyopo eneo la Pugu zote wilaya ya Ilala, Exodus iliyopo Kigamboni na Havard Junior ya wilaya ya Temeke.

Amesema shule nyingine zilizofutwa kabisa ni shule ya sekondari ya Kahe ambayo imefutwa kutokana na wamiliki kushindwa kuiendesha na pia majengo yake yamebadilishiwa matumizi. Alisema shule nyingine za Deogrolius International School iliyopo Kitunda, Desinity na Almustakim zote za jijini Dar es Salaam nazo zimefutiwa usajili. Alisema awali yalitolewa majina ya wamiliki.

Mcheka amesema pia shule mbili hazitakiwi kuwa za bweni ambazo ni Heritage iliyopo Banana Ukonga na Hellens iliyopo Kinondoni.

Akizungumzia shule zilizorejeshewa usajili, alisema ni Gisera, Rose Land, Conerstone na Grace za jijini Dar es Salaam na Must Lead na Qunu zilizopo mkoani Pwani huku shule ya Fountain Gate ikifutiwa usajili wa kuendesha shughuli za bweni.

Akifafanua kuhusu shule ya Coner Stone alisema baada ya ukaguzi na kufutiwa usajili kuanzia mwezi Julai zipo shule ambazo zilikamilisha utaratibu na kurejeshewa usajili, na kwamba hakuna shule iliyoelezwa kufutiwa usajili kwa uongo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *