Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limesema kuwa mkataba wa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji kukodishwa klabu hiyo ni batili.
Tamko hilo limetolewa jana na Kaimu Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja baada ya juzi kusambaa kwa taarifa ya mkataba wa Yanga katika mitandao ya kijamii.
Suala la Yanga kukodishwa timu lilianza mchakato tangu Manji aitishe mkutano mkuu wa dharura miezi miwili iliyopita, akiomba ridhaa ya wanachama wa klabu hiyo kumkodisha timu na nembo kwa miaka 10, ombi ambalo lilipitishwa na kurudishwa katika bodi ya wadhamini kwa ajili ya kufanyiwa kazi na juzi kupitishwa kwa makubaliano hayo.
Kiganja amesema wanaunga mkono suala la mabadiliko, lakini lazima yafuate sheria na taratibu zilizowekwa ili kukamilisha mabadiliko yoyote.
Kiganja alisema hata Bodi ya Yanga iliyohusika kuruhusu timu hiyo kukodishwa haitambuliki kwa Msajili, kwa vile wajumbe wake wengi ni wale waliochaguliwa kwa mpito.
Amesema bodi ya wadhamini iliyoundwa Julai 5, 1973 ni wawili tu wanaotambulika waliopo hadi sasa ambao ni Jabir Katundu na Juma Mwambelo.
Katibu huyo alifafanua taratibu zinazotakiwa kufuatwa ili timu ikodishwe kuwa ni kutumia vikao, ambapo cha kwanza ikiwa ni Kamati ya Utendaji ya Klabu itakayochambua hoja na kukubaliana au kutokukubaliana kisha kupeleka katika kikao cha ngazi za juu.
Pia, amesema baadaye hoja inapelekwa kwenye mkutano mkuu wa wanachama wote uwe wa dharura au kawaida ili kujadiliana hoja husika, kisha baada ya kukubaliana au kutokukubaliana inapelekwa kwa Baraza la wadhamini lenye uwezo wa kuingia kwenye maamuzi makubwa, na mwisho inapelekwa kwa msajili.