Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), ameshindwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kusikiliza kesi ya uchochezi inayomkabili kwa kuwa amekwenda kwenye kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Mbunge wa Mara, Esther Bulaya.
Kutokana na hilo Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alilazimika kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 31, mwaka huu itakapotajwa tena.
Kesi hiyo ilitajwa ili Lissu ajieleze ni kwa nini dhamana yake isifutwe kwa sababu alisafiri kwenda nje ya nchi bila taarifa.
Hakimu Simba amesema dhamana ya washitakiwa wengine katika kesi hiyo ambao ni Mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob inaendelea.
Inadaiwa Januari 12 hadi 14, mwaka huu, Dar es Salaam, Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko Yaja Zanzibar’.
Katika shitaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, mwaka huu, Dar es Salaam, walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.
Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13,mwaka huu katika jengo la Jamana, Ilala, Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi. Aidha alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.