Uongozi wa Yanga umeandika barua kwa serikali ya Zanzibar kuomba kutumia Uwanja wa Amaan kwa ajili ya mechi zake za Ligi Kuu Bara na mashindano mengine.
Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit alisema wamechukua uamuzi huo baada ya Serikali kutangaza kuzifungia Yanga na Simba kutumia Uwanja wa Taifa.
Serikali ilifikia hatua hiyo baada ya mashabiki wa timu hizo kuharibu miundombinu ya uwanja huo, ikiwa ni pamoja na kuvunja mageti na kung’oa viti katika mechi kati yao mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo zilitoka sare ya bao 1-1.
Deusdedit amesema “Tumemwandikia Waziri wa habari, Utamaduni, Utalii na Michezo wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuomba kutumia Uwanja wa Amaan katika mashindano mbalimbali ikiwemo Ligi Kuu Tanzania Bara,”.
Uamuzi wa Yanga kama utakubaliwa timu zitalazimika kusafiri kwenda Zanzibar kuifuata kwa mechi za ligi na zile za kimataifa. Hata hivyo, kanuni za ligi zinaibana Yanga kucheza Zanzibar kwani timu zinatakiwa kuchagua uwanja wa mkoa zinapotoka au mkoa jirani ndani ya Tanzania bara.
Kwa mujibu wa kanuni ya 6 (1-6) za Ligi Kuu bara inaeleza namna ambavyo timu itakavyochagua uwanja wake wa nyumbani na kuitaarifu TFF na bodi ya ligi katika kipindi cha uthibitisho wa ushiriki wa ligi na hatua nyingine ambazo TFF inaweza kuamua kutokana na kuwa na mamlaka ya mwisho.