Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema atafuatilia ili ajue ni kwa nini bidhaa za gypsum (jasi) zinazoagizwa kutoka nje ya nchi hazitozwi kodi zinapoingizwa nchini.

Waziri Mkuu ametoa ahadi wakati akizungumza na watumishi na viongozi wa kiwanda cha Premalt Limited kinachotengeneza unga wa gypsum (jasi) aina ya Afri Bond, mara baada ya kukagua kiwanda hicho kilichopo Zuzu nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Ametumia fursa hiyo pia kumpongeza mmiliki wa Kampuni ya STJ Enterprises, Adella Nungu ambaye ni mmoja wa wajasiriamali wa Kitanzania wanaotumia jasi kutoka Dodoma na kutengeneza mapambo mbalimbali ya kuezekea ndani ya nyumba.

Nungu amesema anaponunua unga wa jasi kutoka Dodoma, kwa wastani anaweza kutengeneza bidhaa za tani 20 hadi 25 kwa mwezi kutegemea na hali ya soko na oda kutoka kwa wateja wake.

Mbali ya kutengeneza mapambo ya kuezekea, unga wa jasi hutumika pia kutengeneza ‘muhogo’ (POP) unaotumika kuwafunga wagonjwa waliovunjika mifupa kama sehemu ya matibabu yao.

Akisoma risala kwa niaba ya uongozi wa Kampuni ya Premalt Limited, Mohammed Mbaraka alisema wamefanya utafiti na kubaini kuwa makontena ya jasi yenye tani zaidi ya 3,000 yanaingizwa nchini bila kutozwa kodi.

Amesema mawe ya madini ya jasi yanachimbwa katika kijiji cha Manda wilayani Chamwino, kilichopo umbali wa kilometa 80 kutoka Dodoma mjini.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Manda, Kambona Matonya alimweleza Waziri Mkuu kwamba kijiji hicho kina wakazi zaidi ya 300 ambao wengi wao wanajishughulisha na uchimbaji wa madini hayo lakini wanakabiliwa na ukosefu wa soko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *